Unicef yataja nchi zenye ukosefu mkubwa wa amani kwa watoto
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umetangaza katika ripoti yake kuwa mustakbali wa mamilioni ya watoto wanaoishi katika nchi zilizokumbwa na vita uko hatarini.
Shirika la Unicef limemetangaza katika ripoti yake hiyo kwamba kuendelea vita katika nchi mbalimbali, kukiukwa haki za watoto na kushindwa viongozi duniani kuwashughulikia wahusika wa jinai hizo kumeuweka hatarini mustakbali wa mamilioni ya watoto.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika kipindi cha miezi 12 ya karibuni watoto wanaoishi Afghanistan, Iraq, Yemen, syria, Myanmar, mashariki mwa Ukraine, Cameroon, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Somalia, Nigeria, Niger, eneo la mpakani mwa Mali na Burkina Faso walikabiliwa na mashambulizi ya moja kwa moja.

Ripoti hiyo ya Unicef imeongeza kuwa watoto wanaoishi kwenye maeneo yaliyokumbwa na mizozo ya kivita wanatumiwa kama ngao ya binadamu, huuawa na hukumbwa na matatizo mbalimbali katika viungo vyao vya mwili.Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa aidha umetahadharisha kuwa watoto wanaoishi katika nchi hizo tajwa wanakabiliwa na masaibu mbalimbali kama njaa na utapiamlo, kushindwa kupata elimu na huduma za afya. Unicef imesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya watoto yanapasa kukomeshwa na haki zao kudhaminiwa.