Qatar yaipa Somalia msaada wa kijeshi, UAE yatengwa
(last modified Fri, 18 Jan 2019 07:34:10 GMT )
Jan 18, 2019 07:34 UTC
  • Qatar yaipa Somalia msaada wa kijeshi, UAE yatengwa

Qatar imeipa Somalia msaada wa kijeshi wa magari 68 ya deraya katika kile ambacho kimetajwa kuwa ni ishara ya kuongezeka ushawishi wa Qatar nchini humo.

Hatua hiyo ya Qatar pia imetajwa kuwa ni ishara ya kuendelea kudhoofika ushawishi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Somalia. Katika taarifa siku ya Alhamisi, Wizara ya Ulinzi ya Qatar imesema magari hayo ya deraya yatakuwa na nafasi muhimu katika kukabiliana na magaidi wakufurishaji wa Al Shabab nchini humo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo Somalia imekataa kupendelea upande wowote katika mgogoro baina ya Qatar na majirani zake yaani Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia, Bahrain pamoja na Misri.

Uhusiano wa UAE na Somalia ulianza kuzorota pale UAE ilipoanza kuwekeza katika eneo lililotangaza kujitenga na Somalia la Somaliland.  Mwezi Aprili, Somalia ilisimamisha mpango wa UAE wa kutoa mafunzo kwa majeshi ya nchi hiyo.

Mwaka jana baadhi ya viongozi wa Umoja wa Afrika waliokuwa wakikutana mjini Addis Ababa Ethiopia waliwasilisha malalamiko rasmi katika Umoja wa Afrika kuhusu hatua ya UAE kuingilia mambo ya ndani ya Somalia.

Nchi hizo za Kiafrika zinasema UAE inahusika katika kuvuruga usalama na uthabiti wa Somalia kwa kuunga mkono magaidi na waasi wanaompinga rais wa sasa wa nchi hiyo Mohamed Abdullahi Mohamed Farmaajo. Wamesema UAE inahasimiana na serikali ya Somalia kwa sababu Rais Farmaajo amepinga sera za Saudi Arabia na UAE za kuhasimiana na Qatar katika mgogoro unaotokota katika Ghuba ya Uajemi.

 

Tags