Feb 11, 2019 14:23 UTC
  • UN: Kusimamishwa Jaji Mkuu wa Nigeria kumekiuka haki za binadamu

Hatua ya kumsimamisha Jaji Mkuu wa Nigeria iliyochukuliwa na rais wa nchi hiyo Muhammadu Buhari imekiuka vipimo vya kimataifa vya haki za binadamu kuhusu uhuru wa vyombo vya mahakama na utenganishaji wa mihimili ya madaraka ya dola.

Hayo yameelezwa na Diego Garcia- Sayan, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na uhuru wa majaji na wanasheria.

Garcia-Sayan amesema, vipimo vya kimataifa vya haki za binadamu vinaeleza kwamba, majaji wanaweza kutimuliwa pale inapotokea kufanya makosa makubwa tu ya kiutendaji na kiuwezo na akaongezea kwa kusema: Uamuzi wowote wa kumsimamisha au kumwondoa jaji katika wadhifa wake inapasa ufanyike kwa uadilifu na utekelezwe na mamlaka huru kama baraza la vyombo vya sheria au mahakama.

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa wa uhuru wa majaji na wanasheria amesisitiza kuwa, kuwafuta kazi majaji bila ya kufuata taratibu za kisheria au kuwapa fursa ya kujitetea dhidi ya uamuzi huo hakuendani na uhuru wa vyombo vya mahakama.

Diego Garcia-Sayan, ripota maalumu wa UN wa uhuru wa majaji na wanasheria

Tarehe 25 ya mwezi uliopita wa Januari, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria alimsimamisha kazi Jaji Mkuu wa nchi hiyo Walter Onnoghen kwa tuhuma za kukiuka sheria na kumteua Ibrahim Tanko Mohammad kujaza nafasi yake.

Buhari amechukua uamuzi huku nchi hiyo ikiwa inajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa rais unaotazamiwa kufanyika siku ya Jumamosi ijayo.

Ikumbukwe kuwa Jaji Mkuu nchini Nigeria ni Rais wa Mahakama ya Juu yenye jukumu la kusikiliza kesi ya kupinga ushindi wa matokeo ya urais.

Ingawa kuna wagombea zaidi ya 70 ambao wamejitokeza kuwania kiti cha urais nchini Nigeria lakini ushindani mkali unatarajiwa kuwa kati ya rais Muhamadu Buhari na mgombea wa chama kikuu cha upinzani PDP Atiku Abubakar aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo.../

 

 

Tags