Miili 24 yatolewa kwenye migodi ya dhahabu nchini Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51608-miili_24_yatolewa_kwenye_migodi_ya_dhahabu_nchini_zimbabwe
Timu ya waokoaji imeopoa maiti 24 kwenye migodi ya dhahabu iliyoporomoka katika mji wa Kadoma, yapata kilomita 145 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Zimbabwe, Harare.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 17, 2019 08:08 UTC
  • Miili 24 yatolewa kwenye migodi ya dhahabu nchini Zimbabwe

Timu ya waokoaji imeopoa maiti 24 kwenye migodi ya dhahabu iliyoporomoka katika mji wa Kadoma, yapata kilomita 145 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Zimbabwe, Harare.

Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya nchi hiyo ZBC, wachimba mgodi wanane wametolewa wakiwa hai kutoka kwenye matimbo mawili ya dhahabu yaliyopomoko siku chache zilizopita.

Hata hivyo timu ya waokoaji imesema yumkini makumi ya wachimba mgodi wamefukiwa kwenye matimbo hayo, yaliyoporomoka Jumanne iliyopita, kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini humo.

Duru za habari zinasema watu kati ya 60 na 70 walifukiwa kwenye migodi hiyo ya dhabahu ilipoporomoka siku ya Jumanne.

Shughuli za uoakoaji timboni

Kutokana na hali ngumu ya maisha, akthari ya wananchi wa Zimbabwe katika maeneo hayo wamekuwa wakichimba migodi ambayo sio salama, kinyume cha sheria.

Hata hivyo wadadisi wa mambo wanavilaumu vyombo vya dola nchini humo, kwa kushindwa kudhibiti shughuli hizo za uchimbaji madini kinyume cha sheria.