Nchi za Magharibi zavunja kimya, zaitaka Algeria iheshimu haki za raia
Nchi za Magharibi zimevunja kimya chao cha muda sasa mbele ya ukandamizaji mkubwa unaofanywa na vyombo vya dola nchini Algeria dhidi ya raia wanaopinga uamuzi wa rais mgonjwa wa nchi hiyo wa kutaka kugombea tena kiti hicho na kuitaka serikali ya Algiers iheshimu haki za raia ikiwemo haki ya kufanya maandamano ya amani.
Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Ulaya imeitaka serikali ya Algeria iheshimu haki ya kujieleza na maandamano ya amani yanayofanyika kote nchini humo ambayo imeyataja kuwa hayajawahi kushuhudiwa tangu baada ya yale yaliyozikumba nchi kadhaa za Kiarabu mwishoni mwa mwaka 2010 na mwanzoni mwa mwaka 2011.
Msemaji wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, katiba ya Algeria inasisitiza haki ya wananchi kujieleza na kufanya mikusanyiko ya amani na kwamba umoja huo unatarajia kwamba, serikali ya Algiers itaheshimu haki hizo na utawala wa sheria.
Wakati huo huo gazeti la New York Times la Marekani limeyataja maandamano yanayofanyika nchini Algeria dhidi ya kiongozi wa nchi hiyo kuwa ndiyo makubwa zaidi kuwahi kushudiwa nchini humo tangu miaka ya thamanini.
Gazeti hilo limemtaka Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria na serikali yake kung'atuka madarakani na kumtaka kiongozi huyo kupata ibra na mafunzo kuhusu hatima ya viongozi wa nchi jirani kama Misri na Tunisia na watu wa familia za watawala wa nchi hizo.
Wapinzani wa kiongozi huyo wanasema, Bouteflika hana uwezo tena wa kuendelea kuongoza nchi kutokana na afya yake kudhoofika na kwa sababu ya kile wanachokiita ufisadi sugu na kukosekana mageuzi ya kiuchumi ya kukabiliana na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kinachopindukia asilimia 25 kwa vijana wenye umri chini ya miaka 30 nchini Algeria.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82, anayetembea kwa kutumia kiti cha magurudumu amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013