Maalim Seif: Inaniuma kukihama Chama cha Wananchi Tanzania CUF
Kinara wa siasa za upinzani visiwani Zanzibar na pia mwanachama namba moja wa chama cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hatua yake ya kuondoka katika Chama cha Wananchi (CUF) imeacha majonzi moyoni mwake.
Maalim Seif ameyasema hayo katika kipindi cha 360 kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds leo Jumatatu na kuongeza kuwa, kwenda kwake ACT-Wazalendo hakukuwa kitendo cha ghafla kwa kuwa, alisoma mazingira na kuyaelewa.
Amefafanua kwa kusema, “Hili jambo halikutokea kwa ghafla, lingetokea kwa ghafla ningeumia zaidi, tulishaona mwendo unavyokwenda. Tuliona dola ina nia ya kumpa chama Prof. Lipumba (Prof. Ibrahim Lipumba), kwa hivyo katika kipindi chote tunavumilia. Tunasikia kuna mpango huu, sisi tukasema tusifanye haraka, kufikia wiki nne kabla tukaona maandishi yako ukutani na kwamba hakuna uwezekano wowote kwa sisi kupewa chama."
Amesema, baada ya kuwepo kwa viashiria vyote kwa Prof. Lipumba kukabidhiwa CUF, waliamua kuanza maandalizi ya kuondoka kwenye chama hicho.
Maalim Seif amebainisha kuwa, “Unaweza kuwa na mke ukaishi naye miaka 20 au 30, ukapata watoto na wajukuu, mwisho wa siku mke akaondoka, utaumia lakini baadaye utazoea tu."
Aidha amesema, uamuzi wa kujiunga na ACT haujavuruga wafuasi wake kwa kuwa, katiba ya chama hicho inafanana na ya CUF na kwamba, hakuna tatizo lolote katika uamuzi wake.
Ameongeza kuwa, yeye pamoja waliokuwa viongozi wa CUF wanashirikiana na uongozi wa ACT-Wazalendo katika kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini Tanzania.