Bunge la Algeria kumteua rais wa mpito baada ya Bouteflika kujiuzulu
Bunge la Algeria linatazamiwa kumteua rais wa mpito atakayeiongoza nchi hiyo baada ya Abdelaziz Bouteflika kujiuzulu.
Shirika rasmi la habari nchini humo APS limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, shuguhuli hiyo ya kumteua rais wa muda atakayerithi mikoba ya Bouteflika kabla ya uchaguzi kuitishwa itafanyika kesho kutwa Jumanne.
Mkuu wa Baraza la Seneti la nchi hiyo, Abdelkader Bensalah ndiye anayetizamiwa kuchukua nafasi hiyo ya kuongoza nchi kwa siku 90 kabla ya kufanyika uchaguzi mpya.
Hata hivyo Bensaleh pamoja na Waziri Mkuu Nouredine Bedoui na Tayeb Belaiz, Mkuu wa Baraza la Katiba aliyepokea barua ya kujiuzulu Boutefika, wanakakabiliwa na mashinikizo ya kujiuzulu pia kutokana kwa wananchi wanaodamana, kwani wanatazwa kama watu waliokuwa karibu na Bouteflikka.
Jumanne iliyopita, Abdelaziz Bouteflika aliyeiongoza Algeria kwa muda wa miaka 20 alikabidhi barua yake ya kujiuzulu urais kwa Baraza la Katiba la nchi hiyo na hivyo kuhitimisha uongozi wake wa miongo miwili katika nchi hiyo.
Mnamo mwezi Februari mwaka huu, Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 na ambaye ni anayugua ugonjwa kiharusi alitangaza kuwa atagombea tena urais kwa muhula wa tano mfululizo.
Kutangazwa habari hiyo kulizusha wimbi la malalamiko makubwa na upinzani mkali wa wananchi na kumfanya kiongozi huyo abadilishe uamuzi wake, ambapo baada ya maandamano mtawalia dhidi yake hatimaye akatangaza kujizulu.