Apr 13, 2019 01:15 UTC
  • UNICEF: Watoto zaidi ya 3,500 wametumika vitani Nigeria tangu 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limesema zaidi ya watoto 3,500 wengi wakiwa na umri wa kati ya miaka 13 hadi 17 waliingizwa na kutumiwa katika vita vinavyoendelea Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na makundi yenye silaha yasiyo ya kiserikali

Katika taarifa hiyo ambayo imetolewa Ijumaa wakati wa kuelekea maadhimisho ya miaka mitano tangu kutekwa kwa watoto wa Chibok nchini Nigeria, UNICEF imetaka kuwepo kwa ulinzi zaidi wa haki za watoto.

Shirika hilo limesema idadi hii ni wale tu ambao wamethibitishwa lakini idadi kamili inaweza kuwa kubwa zaidi. Mbali ya idadi hiyo watoto wengine 432 wameuawa au kujeruhiwa, 180 kutekwa nyara na wasichana 43 kutendewa ukatili wa kingono Kaskazini Mashariki mwa Nigeria mwaka 2018.

Wakati huohuo UNICEFinasema zaidi ya wasichana 100 wa Chibok waliotekwa nyara bado hawajapatikana hadi leo. Maadhimisho ya kutekwa kwa wasicha wa Chibok hufanyika kila Aprili 14 na kwa mujibu wa UNICEF ni kumbusho kwamba utekaji wa watoto na ukiukwaji mkubwa wa haki zao unaendelea Nigeria. Washichana hao walitekwa nyara na kundi la magaidi wakufurishaji wa Boko Haram ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakiendesha uasi Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009.

Hivi sasa kundi hilo limekuwa likiendesha vitendo vya kigaidi katika nchi za Cameroon, Chad, Niger na Nigeria, na mpaka sasa limeshapelekea watu zaidi ya milioni 2.4 kwenye eneo za Ziwa Chad wakimbie makazi yao.

 

Tags