Apr 20, 2019 04:22 UTC
  • Watu 11 wauawa katika shambulio la Boko Haram kaskazini mwa Cameroon

Watu wasiopungua 11 wameuawa kaskazini mwa Cameroon kufuatia shambulio la kundi la kigaidi la Boko Haram.

Duru za karibu na vyombo vya usalama vya Cameroon zinasema kuwa, kundi la Boko Haram limefanya shambulio katika kijiji cha Chakamari cha kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa watu wasiopungua 11.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, makumi ya raia pia wamejeruhi katika shambulio hilo la wanamgambo wa Boko Haram wenye makao yao nchini Nigeria.

Uasi na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram yalianza mwaka 2009 katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria na kisha baadaye kupanua wigo wa mashambulio yake hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Hadi sasa mashambulio hayo yameshasababisha zaidi ya watu elfu ishirini kuuawa na wengine karibu milioni tatu kubaki bila makazi na hivyo kulazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria.

Itakumbukwa kuwa, kundi la kigaidi la Boko Haram la Nigeria lilitangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh mwaka 2014.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amekuwa akiahidi kila mara kuchukua hatua kali za kupambana na kuliangamiza kundi la kigaidi la Boko Haramu, lakini hadi sasa ameshindwa kutimiza ahadi yake hiyo, na hivyo kukabiliwa na ukosoaji wa ndani na nje.

Tags