Waandamanaji Algeria wataka kupandishwa kizimbani ndugu ya Bouteflika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53111-waandamanaji_algeria_wataka_kupandishwa_kizimbani_ndugu_ya_bouteflika
Wananchi wa Algeria jana waliandamana tena ikiwa ni Ijumaa ya 10 mtawalia ya maandamano yao ambapo mbali na kusisitiza juu ya kuachia ngazi viongozi na maafisa wote wa serikali waliokuwa katika kipindi cha utawala wa Abdelaziz Bouteflika, Rais wa nchi hiyo aliyelazimika kujiuzulu, wametoa mwito wa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria Said Bouteflika, ndugu ya rais huyo mkongwe aliyejiuzulu kufuatia maandamano ya wananchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 26, 2019 22:11 UTC
  • Waandamanaji Algeria wataka kupandishwa kizimbani ndugu ya Bouteflika

Wananchi wa Algeria jana waliandamana tena ikiwa ni Ijumaa ya 10 mtawalia ya maandamano yao ambapo mbali na kusisitiza juu ya kuachia ngazi viongozi na maafisa wote wa serikali waliokuwa katika kipindi cha utawala wa Abdelaziz Bouteflika, Rais wa nchi hiyo aliyelazimika kujiuzulu, wametoa mwito wa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria Said Bouteflika, ndugu ya rais huyo mkongwe aliyejiuzulu kufuatia maandamano ya wananchi.

Waandamanaji hao wanamtuhumu Said Bouteflika kuwa 'kiongozi wa genge' la ufisadi lililopora mali za nchi hiyo. Ndugu watatu wanaotajwa kuwa matajiri zaidi nchini humo na wapambe wa karibu wa Said Bouteflika walitiwa mbaroni siku chache zilizopita kwa ajili ya kusailiwa, wakihusishwa na kashfa za ufisadi.

Wananchi hao wa Algeria katika mji mkuu wa nchi hiyo Algiers jana Ijumaa walitangaza kwamba, wanataka viongozi na maafisa wote wa serikali ya Bouteflika kujiuzulu nafasi zao za uongozi.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao yalikuwa yameandikwa "Mfumo wote lazima uondoke, tumechoka na nyinyi."

Licha ya maafisa usalama kupelekwa katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Algiers, lakini hilo halikuwazuia waandamanaji kujitokeza kwa wingi hapo jana

Tarehe 2 Aprili, Abdelaziz Bouteflika alitangaza rasmi  kujiuzulu wadhifa wa Urais baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miongo miwili, kufuatia maandamano makubwa ya upinzani ya kupinga serikali yaliyofanyika kwa wiki sita mtawalia nchini Algeria.

Rais wa muda wa Algeria, Abdelkader Bensalah alitangaza hivi karibuni kwamba, tarehe 4 Julai mwaka huu ndiyo siku ya kufanyika uchaguzi wa kumtafuta mrithi wa Abdelaziz Bouteflika, rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu.