Maandamano ya wananchi yaendelea Algeria kupinga serikali ya mpito
Wananchi wa Algeria wameendelea na maandamano yao ya kupinga serikali ya mpito ya nchi hiyo na kuishutumu kuwa inapoteza muda.
Katika maandamano yao ya jana, waandamanaji nchini Algeria wamesema kuwa, pendekezo la Abdelkader Bensalah, mkuu wa serikali ya mpito ya nchi hiyo la kutaka kufanyike mazungumzo baina ya serikali na waandamanaji ni kupoteza muda.
Waandamanaji hao wameendelea na maandamano yao wakiwa wamebeba bendera za nchi yao na kuwataka Abdelkader Bensalah na waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Algeria, Noureddine Bedoui wajiuzulu na kukabidhi madaraka hasa kwa kuzingatia kuwa wawili hao ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa serikali ya Abdelaziz Boutefliqa iliyong'olewa madarakani na maandamano ya wananchi.
Lengo la waandamanaji hao katika Ijumaa ya 11 ya maandamano yao ya amani ni kuwang'oa uongozini viongozi wote wa serikali iliyopita.
Ni vyema tukaashiria hapa kuwa, uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika tarehe 14 Julai mwaka huu. Hata hivyo wapinzani wanaamini kwamba wakati wa kufanyika uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia haujafika kwani kuna mambo mengi ya kurekebishwa na kuna mianya mingi ya kuzibwa kabla ya kufanyika uchaguzi huo.