Watu kadhaa wauawa katika machafuko mapya nchini Sudan
(last modified Tue, 14 May 2019 07:45:44 GMT )
May 14, 2019 07:45 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika machafuko mapya nchini Sudan

Sambamba na kuanza duru mpya ya mazungumzo kuhusiana na suala la kukabidhiwa madaraka ya Sudan kwa utawala wa kirai jana Jumatatu, imearifiwa kuwa watu sita wakiwemo maafisa usalama wameuawa au kujeruhiwa katika machafuko mapya yaliyoibuka katika mji mkuu Khartoum jana jioni.

Kanali ya televisheni ya serikali  imetangaza kuwa, makundi ya watu wasiojulikana yamewashambulia waandamanaji mjini Khartoum, na kusababisha kifo cha afisa mmoja wa usalama na raia watatu, mbali na watu wengine kadhaa kujeruhiwa. Milio ya risasi imesikika usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu huo. 

Haya yanajiri licha ya Baraza la Mpito la Kijeshi nchini humo kutangaza kuwa limefikia makubaliano na muungano wa upinzani kuhusu muundo na mfumo wa serikali ya mpito. Baraza hilo limesema kuna baadhi ya vyama vinavyolenga kuvuruga makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya jana ndiposa vikaanzisha ghasia.

Viongozi wa maandamano nchini Sudani wamekuwa wakilituhumu Baraza la Mpito la Kijeshi nchini humo kwamba, linapoteza muda na hivyo kuchelewesha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Waandamanaji wa Sudan wanaotaka madaraka yakabidhiwe raia

Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Jenerali Omar Hassan al Bashir.

Wapinzani nchini Sudan wanasisitiza kuwa, madhali Baraza la Mpito la Kijeshi halijakabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia maandamano na malalamiko ya wananchi wa nchi hiyo yataendelea kushuhudiwa.