Libya katika ncha ya kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53641-libya_katika_ncha_ya_kutumbukia_kwenye_vita_vya_wenyewe_kwa_wenyewe
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ameonya kuwa, taifa hilo lenye utajiri wa mafuta liko katika ncha ya kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vitaigawa nchi hiyo mapande mapande.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2019 03:26 UTC
  • Libya katika ncha ya kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ameonya kuwa, taifa hilo lenye utajiri wa mafuta liko katika ncha ya kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vitaigawa nchi hiyo mapande mapande.

Ghassan Salame ameyasema hayo katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, makundi ya kigaidi ya Daesh (ISIS) na al-Qaeda yanatumia ombwe la usalama lililosababishwa na mapigano baina ya vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar na Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa, kujihuisha na kujiimarisha. 

Amesema bendera nyeusi za ISIS zinapepea kusini mwa Libya, na kwamba genge hilo la ukufirishaji limefanya mashambulizi manne tokea Jenerali Haftar aanzishe vita hivyo mnamo Aprili 4, na kwamba watu wasiopungua 17 wameuwa katika hujuma hizo.

Amesema, "Vikosi vya Libya huko nyuma vilipambana kwa ujasiri kuzima harakati za magenge ya kigaidi, lakini hivi sasa vinapambana vyenyewe kwa vyenyewe. 

Jenerali muasi Haftar alianzisha vita muda mfupi baada ya kuitembelea Saudia

Mapigano hayo yanaendelea licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mapema mwezi huu kutoa mwito wa kusitishwa mapigano hayo, huku likiziasa pande husika kurejea katika meza ya mazungumzo.

Zaidi ya watu 460 wameuawa na wengine 240 kujeruhiwa, tokea Aprili 4 wakati wapiganaji wa Haftar walipoanza kuuhujumu mji wa Tripoli. Jenerali muasi Khalifa Haftar amepuuzilia mbali wito wa kimataifa unaomtaka asitishe mapigano dhidi ya wapiganaji watiifu kwa serikali ya Libya yenye makao yake mjini Tripoli na inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.