Hofu ya UN kuhusu kifo cha mwanaharakati wa upinzani Gambia
"Kifo cha kiongozi wa upinzani aliyekuwa kizuizini nchini Gambia lazima kichunguzwe na kuwapa tiba majeruhi waliokuwa wakiandamana kwa amani ambao bado wako kizuizini", amesema Kamisha Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa yake baada ya kifo cha mjumbe wa chama cha United Democratic (UDP) Solo Sandeng, mmoja wa wanaharakati watatu waliouawa baada ya maandamano ya wiki iliyopita, Zeid Ra’ad Al Hussein amesema hali hiyo inasikitisha sana na inaashiria mazingira ya hofu kabla ya uchaguzi nchini Gambia.
Duru zinasema vikosi vya usalama vilivunja maandamano ya amani wiki iliyopita na kujeruhi vibaya watu wengi. Kwa mujibu wa Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu, kuna wasiwasi kuhusu muandamanaji ambaye bado yuko kizuizini na anahitaji msaada wa haraka wa tiba.
Ameongeza kuwa kufuatia kifo cha kiongozi huyo wa upinzani kumekuwepo maandamano mapya, na kuna hofu kuhusu jinsi serikali itakavyowachukulia hatua wakati huu hali ya haki za binadamu ikizidi kuwa mbaya.
Makumi ya raia wametiwa mbaroni nchini Gambia katika maandamano yaliyofanyika Ijumaa ya kumpinga Rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo.
Maandamano hayo yalikandamizwa na askari usalama huku makumi ya waandamanaji wakitiwa mbaroni. Habari kutoka Gambia zinasema kuwa, maandamano hayo ni makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.
Waandamanaji, wakiwa wamebeba mabango na maberamu, walipiga nara wakipinga sera za Rais huyo na kutoa wito wa kufanyika mageuzi ya kisiasa.
Rais Jammeh anaongoza Gambia kwa mkono wa chuma tangu mwaka 1994.