Tunisia na Niger zachaguliwa kuwa wanachama wa Baraza la Usalama
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Ijumaa lilizichagua nchi tano wanachama wa umoja huo kuwa wanachama wasio wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuanzia mwezi Januari mwakani.
Uchaguzi huo umefanyika kwa mujibu wa Ibara ya 23 ya Katiba ya Umoja wa Mataifa na kanuni namba 142 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu chaguzi za kila mwaka za wajumbe wasio wa kudumu wa baraza hilo ambao watahudumu kwa kipindi cha miaka miwili.
Kanuni zinamtaka mshindi apate theluthi mbili za kura ambapo mara hii kwa upande wa bara la Afrika, nchi zilizochaguliwa ni Niger na Tunisia ambazo zitachukua nafasi ya Cote d’Ivoire na Equatorial Guinea zinazomaliza muda wao mwishoni mwa mwaka huu.
Kutoka kundi la Asia-Pasifiki, kiti kilichokuwa kinashindaniwa ni kimoja ambapo Vietnam imeshinda na itachukua nafasi ya Kuwait.
Kwa upande wa kundi la nchi za Amerika ya Kusini na Karibea, Saint Vincent na Grenadines imeibuka kidedea kwa kupata kura 185 dhidi ya El Salvador iliyopata kura 6 na hivyo kuchukua nafasi ya Peru inayomaliza muda wake. Nchi ya Saint Vincent na Grenadines imeweka rekodi kama nchi ndogo zaidi duniani kuwahi kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama.
Nafasi ya bara la Ulaya imechukuliwa na Estonia iliyopata kura 132 ambayo imezishinda nchi nyingine tatu ambazo ni Romania, Georgia na Latvia na sasa Estonia itachukua nafasi ya Poland inayomaliza muda wake.
Baraza la Usalama lina jumla ya wanachama 15 ambapo 10 wasio wa kudumu hivi sasa ni Ubelgiji, Cote d’Ivoire, Equatorial Guinea, Jamhuri ya Dominika, Ujerumani, Indonesia, Kuwait, Peru, Poland na Afrika ya Kusini. Wanachama wa kudumu ni Uingereza, Ufaransa, China, Urusi na Marekani.
Kwa muda sasa kumekuwepo na maombi ya kutaka kuwepo mabadiliko katika muundao wa Baraza la Usalama ili kuongeza wanachama wa kudumu huku bara la Afrika likisema ni haki yake kuwa na kiti cha kudumu katika baraza hilo ili nalo liweze kuwa na kura ya turufu kama mabara mengine.