Mtaalamu wa UN aondoka Comoro baada ya kuzuiwa kufanya kazi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54205-mtaalamu_wa_un_aondoka_comoro_baada_ya_kuzuiwa_kufanya_kazi
Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu utesaji, Nils Melzer, amesitisha ziara yake aliyokuwa afanye Comoro, baada ya kukumbwa na vizuizi kadhaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 18, 2019 22:09 UTC
  • Mtaalamu wa UN aondoka Comoro baada ya kuzuiwa kufanya kazi

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu utesaji, Nils Melzer, amesitisha ziara yake aliyokuwa afanye Comoro, baada ya kukumbwa na vizuizi kadhaa.

Ziara hiyo ya wiki moja ililenga kutoa fursa kwa mtaalamu huyo kutathmini na kubaini changamoto juu ya hatua za kuzuia utesaji na aina nyingine ya ukatili pamoja na adhabu zisizo za kiutu.

Taarifa iliyotolewa Jumanne na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCRC, imemnukuu Melzer akielezea masikitiko yake kuwa alishindwa kufikia kwa uhuru watu wote ambao alihisi ni muhimu ili kukamilisha jukumu lake.

Mathalani, Melzer aliweza kufanya ziara aliyopanga kwenye rumande moja huko Comoro Kuu lakini ziara yake kwenye maeneo matatu yaliyo chini ya polisi na mahakama huko Moroni na kisiwa cha Anjouan zilizuiliwa.

Anasema kuzuiwa kwake kunatia hofu sana kwa sababu alikuwa amepokea ushahidi mahususi wa madai ya vitisho, matumizi ya nguvu kupita kiasi na watuhumiwa kutendewa maovu. 

Mtaalamu huyo amesema wiki ijayo atawasilisha ripoti yake ya awali na kwamba ataendelea kuwasiliana na serikali ya Comoro na wasuluhishi huku akisema ripoti yake kamili ataiwasilisha mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwakani.

Kiongozi wa upinzani Comoro Ahmed Abdallah Mohamed Sambi ambaye anaendelea kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria

Comoro imekuwa katika mgogoro wa kisiasa kwa muda mrefu sasa huku wapinzani wakilalmikia vikali ukandamizaji unaotekelezwa na utawala wa nchi hiyo.

Mwezi Aprili Mahakama ya Katiba nchini Comoro ilithibitisha ushindi wa Rais Azali Assoumani baada ya kupata asilimia 59 ya kura zote, katika uchaguzi wa urais uliofanyika Machi na ambao ulilalamikiwa na mrengo wa upinzani.

Mwaka jana Rais Azali Assoumani alishinda kura ya maoni ya marekebisho ya katiba  ya kurefusha kipindi cha uongozi wa rais na kukomesha mfumo wa kuongoza kwa zamu baina ya visiwa vitatu vikuu vinavyounda Jamhuri ya Watu wa Comoro, jambo ambalo limeibua mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini humo.