Jun 19, 2019 07:34 UTC
  • Magaidi waua wanajeshi 15 kaskazini mwa Nigeria

Wanajeshi 15 wa Nigeria wameuawa katika shambulizi linaloaminika kutekelezwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi.

Afisa wa jeshi ambaye hakutaka jina lake litajwe bila maelezo zaidi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, kufikia sasa wameweza kupata maiti 15 za wanajeshi hao waliouawa. Jeshi la Nigeria halijatoa taarifa rasmi kuhusu mauaji hayo kufikia sasa.

Mauaji hayo ya usiku wa kuamkia jana yamejiri siku moja baada ya watu wasiopungua 30 kuuawa katika mashambulizi ya kigaidi kaskazini mwa Nigeria katika hujuma inayoaminika kutekelezwa na magaidi wakufurishaji wa Boko Haram.

Kwa mujibu wa taarifa, magaidi watatu waliokuwa wamejifunga mikanda ya mabomu walijilipua Jumapili usiku katika ukumbi wakati watu walipokuwa wakitizama mechi ya soka kwa njia ya televisheni, katika eneo la Konduga, kilomita 38 kutoka mji mkuu wa jimbo la Borno, Maiduguru.  

Magaidi wa Boko Haram wanaofanya mauaji ya kutisha dhidi ya raia na mafisa usalama Afrika Magharibi

Mauaji hayo ya usiku wa kuamkia jana aidha yanaripotiwa chini ya wiki moja baada ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika eneo la Magharibi mwa Afrika (ISWA) kudai kwamba limeua askari 20 wa Nigeria katika mji wa Kareto, katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi.

Tangu mwaka 2009 hadi sasa, kundi la kigaidi la Boko Haram limeua watu zaidi ya elfu 20 katika nchi za Nigeria, Niger, Chad, na kaskazini mwa Cameroon na kuwafanya wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi. 

Tags