Jul 05, 2019 02:55 UTC
  • Pande hasimu za Sudan zakubaliana kugawana madaraka

Wawakilishi wa Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan na muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko wameafikiana juu ya suala la kugawana madaraka katika kipindi cha mpito kuelekea katika uchaguzi.

Muafaka huo ni matunda ya mazungumzo ya moja kwa moja ya siku mbili mjini Khartoum, juu ya kipindi cha mpito na idadi ya wawakilishi wa kila upande katika baraza la uongozi la kipindi hicho cha mpito.

Kikao kilichofanyika juzi na jioni ya jana kinahesabiwa kuwa cha kwanza cha ana kwa ana baina ya pande hizo mbili baada ya mauaji ya makumi ya waandamanaji mjini Khartoum hapo tarehe 3 mwezi uliopita wa Juni; na kimehudhuriwa na mpatanishi wa Umoja wa Afrika, Mohamed Hacen El Lebatt na yule wa Ethiopia Mahmud Dirir.

Mjumbe wa AU Hacen El Lebatt amesema baada makubaliano hayo kuwa, "Pande mbili zimeafikiana kuunda baraza huru la mpito na la kiduru kati ya jeshi na raia ambalo litadumu kwa muda miaka mitatu au zaidi, kuelekea uchaguzi mkuu."

Mazungumzo ya Khartoum

Maelfu ya wananchi walimiminika mabarabarani hiyo jana katika mji mkuu Khartoum na mji wa Omdurman ulioko karibu na Mto Nile baada ya kuibuka habari ya makubaliano hayo. Aidha pande mbili zimekubaliana kuunda jopo huru litakalochunguza vitendo vya ghasia na mauaji ya hivi karibuni.

Jumapili iliyopita, Baraza la Kijeshi la Mpito lilikabiliana kwa mkono wa chuma na maandamano ya wananchi, ambapo watu 11 waliuawa na wengine zaidi ya 180 kujeruhiwa.

Tags