Rais wa Nigeria aonywa kuhusu hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54633-rais_wa_nigeria_aonywa_kuhusu_hali_ya_kiafya_ya_sheikh_zakzaky
Wanachama kadhaa wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wamemuonya rais wa nchi hiyo kuhusu hali mbaya ya Kiafya ya kiongozi wa harakati hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2019 07:00 UTC
  • Rais wa Nigeria aonywa kuhusu hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky

Wanachama kadhaa wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wamemuonya rais wa nchi hiyo kuhusu hali mbaya ya Kiafya ya kiongozi wa harakati hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Kwa mujibu wa Press TV, onyo hilo limetolewa leo na wanachama hao wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wakisema kuwa, kama baya lolote litamtokea Sheikh Ibrahim Zakzaky basi lawama zote zitakwenda kwa Rais Muhammadu Buhari.

Familia ya Sheikh Zakzaky inasema kuwa, hali ya kiafya ya kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu si nzuri hata kidogo na hali hiyo inazidi kuwa mbaya, siku baada ya siku.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inashinikiza kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe hasa kutokana na Mahakama Kuu ya nchi hiyo kutoa amri ya kuachiliwa huru. 

Hali ya Sheikh Ibrahim Zakzaky imeripotiwa kuwa mbaya, lakini serikali hairuhusu akatibiwe nje ya nchi

 

Sheikh Zakzaky na mkewe walipigwa risasi na jeshi la Nigeria tarehe 13 Disemba 2015 katika Husainia ya Harakati ya Kiislamu huko Zaria.

Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru mara moja mwanachuoni huyo mwezi Disemba 2016, kama ambavyo lililiwajibisha jeshi la nchi hiyo kuilipa fidia ya dola laki moja na 50 elfu familia ya Sheikh Zakzaky. Hata hivyo jeshi, serikali na vyombo vya dola vimekataa kutekeleza amri hiyo ya mahakama, na hadi hivio sasa kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu anaendelea kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria.