Baraza la Taifa la Nigeria laahidi kufuatilia faili la Sheikh Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54650-baraza_la_taifa_la_nigeria_laahidi_kufuatilia_faili_la_sheikh_zakzaky
Baraza la Taifa la Nigeria limetangaza kuwa, lina mpango wa kufuatilia faili la Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anayeshikiliwa kororoni kwa miaka kadhaa sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2019 06:54 UTC
  • Baraza la Taifa la Nigeria laahidi kufuatilia faili la Sheikh Zakzaky

Baraza la Taifa la Nigeria limetangaza kuwa, lina mpango wa kufuatilia faili la Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anayeshikiliwa kororoni kwa miaka kadhaa sasa.

Tangazo hilo la Baraza la Taifa la Nigeria linakuja kufuatia kushadidi malalamiko na maandamano ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky na baada ya kutangazwa habari ya kuzidi kuwa mbaya afya ya mwanaharakati huyo wa Kiislamu.

Taarifa ya Baraza la Taifa la Nigeria imesisitiza kuwa, chombo hicho kitaingilia kati na kufuatilia faili la Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Aidha hatua ya Baraza la Taifa la Nigeria inakuja siku chache tu baada ya Muhammad Ibrahim, mtoto wa Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria kutahadharisha kupitia ujumbe aliotoa kwamba hali ya kimwili ya baba yake ni mbaya sana na kwamba, karibu njia zote za kutaka kunusuru maisha yake zimeshindikana.

Maandamano ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky

Wakati huo huo, chunguzi mpya za kitiba zimethibitisha kuwa, katika damu ya Sheikh Zakzaky kuna mada za sumu ya risasi na cadmium; jambo linaloonyesha kuwa sumu hiyo alipewa akiwa jela.

Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru mara moja mwanachuoni huyo mwezi Disemba 2016, kama ambavyo ililiwajibisha jeshi la nchi hiyo kuilipa fidia ya dola laki moja na 50 elfu familia ya Sheikh Zakzaky. Hata hivyo jeshi, serikali na vyombo vya dola vimekataa kutekeleza amri hiyo ya mahakama, na hadi hivi sasa mwanaharakati huyo wa Kiislamu anaendelea kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria.