Jeshi la Nigeria laendelea kumwaga damu za wafuasi wa Zakzaky
Mtu mmoja ameuawa na maafisa usalama katika mji wa Kano nchini Nigeria wakati wa maandamano makubwa ya kushinikiza kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anayeshikiliwa korokoroni kwa miaka kadhaa sasa.
Kadhalika watu wawili wamejeruhiwa vibaya baada ya jeshi la Nigeria kuwamiminia risasi wafuasi wa Sheikh Zakzaky katika maandamano hayo ya jana Jumanne.
Waandamanaji hao wa Kano ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Nigeria huko magharibi mwa Afrika walisikika wakipiga nara za kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Aidha waandamanaji hao wamesisitiza kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky anaendelea kushikiliwa kinyume cha sheria, hivyo vyombo vya usalama vinapaswa kutii amri ya mahakama na kumuachiliwa huru mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
Jumapili iliyopita pia, maafisa usalama walitumia risasi hai na mabomu ya kutoa machozi kuvunja maandamano ya amani ya wananchi katika mji huo wa Kano, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa.
Aidha siku chache zilizopita, vikosi vya usalama nchini Nigeria vilitumia risasi za vita dhidi ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky katika miji ya Abuja na Kaduna, ambapo watu watatu akiwemo mtoto mdogo waliuawa, mbali na makumi ya wengine kukamatwa.
Sheikh Zakzaky na mkewe walitiwa mbaroni tarehe 13 Disemba 2015 katika Huseiniya ya Harakati ya Kiislamu huko Zaria kufuatia shambulio la jeshi la nchi hiyo lililoua shahidi mamia ya Waislamu wasio na hatia, na serikali imepuuza agizo lilitolewa na Mahakama Kuu ya nchi hiyo mwaka 2016 la kutaka msomi huyo wa Kiislamu aachiwe huru.