Waandamanaji wanne wauawa katika mji wa Omdurman nchini Sudan
Waandamanaji wanne wanaripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi katika maandamano yaliyofanyika jana katika mji wa Omdurman huko nchini Sudan, huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.
Mauaji hayyo yametokea katika hali ambayo, wawakilishi wa baraza la kijeshi linalotawala Sudan na wa muungano mkuu wa upinzani waliripotiwa kupiga hatua katika masuala yenye mvutano kwenye mazungumzo ya kipindi cha mpito kutoka utawala wa kijeshi kuelekea utawala wa kiraia.
Maandamano kama hayo yamefanyika pia katika mji mkuu wa Sudan Khartoum yakilishinikiza Baraza la Mpito la Kijeshi nchini humo likabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.
Mauaji ya jana ya vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji yamelaaniwa vikali na wapinzani nchini Sudan ambao wamesisitiza kwamba, kuna haja ya kuwajibishwa wale waliohusika na mauaji hayo.
Itakumbukwa kuwa, wanafunzi sita waliuliwa kwa kupigwa risasi siku ya Jumatatu wakati askari usalama wa Sudan walipokuwa wakiwatawanya wanafunzi hao walioandamana kulalamikia uhaba wa mafuta na mikate katika mji wa El-Obeid, mkoani Kordofan Kaskazini.
Baraza la Kijeshi la Uongozi wa Mpito la Sudan lilichukua hatamu za uongozi baada ya jeshi kufanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Rais Omar al Bashir Aprili 11 mwaka huu; hata hivyo wananchi wangali wanaandamana wakishinikiza kuundwa serikali ya kiraia huko Sudan.