IMN: Serikali ya Nigeria inataka kumuua Sheikh Ibrahim Zakzaky
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeashiria ukwamishaji matibabu uliofanywa na viongozi wa serikali ya Nigeria dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky alipokuwa nchini India na kueleza kwamba, hatua hizo zimeibua dhana kwamba, serikali ya Abuja inafanya njama za kumuua mwanaharakati huyo.
Taarifa iliyotolewa na harakati hiyo baada ya Sheikh Ibrahim Zakzaky kurejea Nigeria imeeleza kwamba, uingiliaji wa serikali ya Nigeria na njama zake za kukwamisha mwenendo wa matibabu wa Sheikh Zakzaky umeibua dhana hii kwamba, serikali ya Abuja inataka kumuua kiongozi huyo kupitia baadhi ya watu wake wa kigeni.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeashiria njama za serikkali ya Nigeria za kutaka kumpa sumu na kumuua Sheikh Zakzaky alipokuwa korokoroni na kueleza kwamba, kutokana na kutokuwa na imani na serikali ya Abuja, Sheikh Zakzaky alichagua Shirika la Ndege la Kigeni kwa ajili ya safari yake ya kuelekea India.
Kadhaliika taarifa hiyo imebainisha kwamba, Sheikh Zakzaky amelazimika kurejea Nigeria baada ya kupoteza imani yake na mwenendo mzima wa matibabu hasa baada ya madaktari wake binafsi kuzuiwa kushughulikia faili la matibabu yake.
Taarifa zaisi zinasema kuwa, kutokuwepo suhula, vifaa visivyofaa vya matibabu, kutokuwepo madaktari wa kuaminika, kuzuiliwa hospitalini na kisha mashinikizo ya serikali ya Nigeria ya kuitaka India imfukuze kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, ni mambo yaliyomlazimisha Sheikh Zakzaky kuchukua uamuzi wa kuondoka India na kurejea Nigeria.