Wananchi wa Algeria waandamana wakitaka kutimuliwa mabaki ya utawala wa Bouteflika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55570-wananchi_wa_algeria_waandamana_wakitaka_kutimuliwa_mabaki_ya_utawala_wa_bouteflika
Maelfu ya wananchi wa Algeria wameendelea na maandamano yao ya nchi nzima kushinikiza kufukuzwa serikalini mabaki yote ya utawala wa Abdulaziz Bouteflika, rais wa nchi hiyo aliyelazimika kujiuzulu kutokana na maandamano makubwa ya wananchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 24, 2019 07:39 UTC
  • Wananchi wa Algeria waandamana wakitaka kutimuliwa mabaki ya utawala wa Bouteflika

Maelfu ya wananchi wa Algeria wameendelea na maandamano yao ya nchi nzima kushinikiza kufukuzwa serikalini mabaki yote ya utawala wa Abdulaziz Bouteflika, rais wa nchi hiyo aliyelazimika kujiuzulu kutokana na maandamano makubwa ya wananchi.

Wananchi wa Algeria jana waliendelea na maandamano yao ya kila wiki ikiwa ni Ijumaa ya 27 mfufulizo wakipiga nara za kulaani majenerali wa kijeshi na kuwataka waache kuwaunga mkono na kuwasaidia mabaki ya utawala wa Abdulaziz Bouteflika.

Waandamanaji hao wanataka pia kutiwa mbaroni na kupandishwa kizimbani watu wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

Kadhalika wananchi hao wanaitaka  serikali ya mpito ya nchi hiyo kusikiliza matakwa yao sambamba na kulaani njama zote zenye lengo la kuvuruga umoja na mshikamano wa nchi hiyo.

Vilevile waandamanaji hao wanataka kuhudhuria watu wenye ustahiki katika mazungumzo ya kitaifa na kuitishwa uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo haraka iwezekanavyo.

Abdelkader Bensalah, Kaimu Rais wa Algeria ambaye pia ni Spika wa Bunge la nchi hiyo

Itakumbukwa kuwa, tarehe pili Aprili mwaka huu, Abdelaziz Bouteflika alilazimika kuachia madaraka ya Algeria baada ya kushadidi maandamano ya wananchi dhidi ya utawala wake.

Madaraka ya Algeria hivi sasa yako mikononi mwa Abdelkader Bensalah, Spika wa Bunge la nchi hiyo ambaye anaongoza serikali ya mpito hadi baada ya siku 90 utakapoitishwa uchaguzi mkuu nchini humo.

Katika miezi ya hivi karibuni, mahakama ya Algeria imeanzisha uchunguzi kuhusu ufisadi wa viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Bouteflika ambaye uongozi wake ulianza mwaka 1999 na kuhitimishwa na maandamano ya wananchi Aprili mwaka huu.