Watu 10 wafariki, 98 wajeruhiwa kwenye msongamano wa kampeni za uchaguzi Msumbiji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55973-watu_10_wafariki_98_wajeruhiwa_kwenye_msongamano_wa_kampeni_za_uchaguzi_msumbiji
Watu wasiopungua 10 wamefariki dunia nchini Msumbiji na wengine 98 wamejeruhiwa katika vurugu na msongamano uliotokea katika mkutano wa kampeni za uchaguzi uliohutubiwa na rais wa nchi hiyo Filipe Nyusi.
(last modified 2026-01-05T06:17:05+00:00 )
Sep 13, 2019 07:23 UTC
  • Watu 10 wafariki, 98 wajeruhiwa kwenye msongamano wa kampeni za uchaguzi Msumbiji

Watu wasiopungua 10 wamefariki dunia nchini Msumbiji na wengine 98 wamejeruhiwa katika vurugu na msongamano uliotokea katika mkutano wa kampeni za uchaguzi uliohutubiwa na rais wa nchi hiyo Filipe Nyusi.

Mamlaka za hospitali nchini Msumbiji zimeripoti kuwa, watu hao walifariki na kujeruhiwa wakati umati mkubwa wa watu ulipojaribu kupita kwenye lango moja tu la uwanja wa michezo wa Nampula, kaskazini mwa nchi ulikokuwa ukifanyika mkutano huo wa kampeni siku ya Jumatano. Watu hao walibinywa na kukanyagwa walipokuwa wakijaribu kutoka uwanjani humo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari hapo jana, Mkurugenzi wa hospitali ya mji huo Cachimo Molina alisema, watu 98 walilazwa hospitalini kwa ajili ya uangalizi na kwamba ukiondoa 14, wengine wote kati yao baadaye waliruhusiwa kurudi majumbani. Majeruhi wanane wako kwenye kitengo cha uangalizi maalumu.

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji Basilio Monteiro ametangaza kuundwa tume maalumu ya kuchunguza chanzo na sababu ya kujiri tukio hilo.

Msumbiji iko kwenye wiki ya pili ya kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 15 ya mwezi ujao wa Oktoba, ambapo rais Nyusi anayewania kiti hicho kwa tiketi ya chama tawala Frelimo anatazamiwa kushinda na kuiongoza tena nchi hiyo kwa muhula mwingine wa pili.

Kwa mujibu wa Kituo cha Utangamano wa Umma, watu 12 walifariki katika wiki ya mwanzo ya kampeni za uchaguzi wakiwemo 10 waliofariki kwenye ajali za barabarani na wawili katika machafuko ya kisiasa. Watu wengine 27 walijeruhiwa, ambapo 16 katika ajali za barabarani na 13 katika machafuko ya kisiasa.../