Waafrika Kusini wajiunga na wageni katika maandamano ya kulaani 'xenophobia'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56014-waafrika_kusini_wajiunga_na_wageni_katika_maandamano_ya_kulaani_'xenophobia'
Wananchi wazalendo wa Afrika Kusini wamejiunga na raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini humo, katika maandamano ya kulaani ghasia na mauaji yanayowalenga raia wa kigeni hususan Waafrika wanaoishi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 15, 2019 07:20 UTC
  • Waafrika Kusini wajiunga na wageni katika maandamano ya kulaani 'xenophobia'

Wananchi wazalendo wa Afrika Kusini wamejiunga na raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini humo, katika maandamano ya kulaani ghasia na mauaji yanayowalenga raia wa kigeni hususan Waafrika wanaoishi nchini humo.

Gabriel Hertis, mratibu wa Jumuiya ya Waafrika Wanaoishi Afrika Kusini (Social Cohesion from the Africa Diaspora Forum) ambaye ni mzaliwa wa Rwanda amesema lengo la mashirika mbalimbali kuandaa na kushiriki katika maandamano hayo yaliyofanyika jana mjini Johannesburg, ni kukosoa kwa kauli moja hujuma dhidi ya wageni nchini humo.

Naye Mwenyekiti wa Jamii ya Wazimbabwe Wanaoishi Afrika Kusini, Ngqabutho Mabhena sanjari na kulaani jinai hizo ameeleza bayana kuwa, "Tupo hapa ili kuwafahamisha raia wa nchi hii kwamba uhajiri ni kadhia ya kimataifa, ambapo tunapaswa kuishi pamoja kwa amani kama Waafrika. Pia tunataka kuwahamiza wahajiri wenzetu kuwa wana wajibu wa kutii sheria za nchi hii."

Kwa upande wake, Rais wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini humo (GIWUSA), Mametlo Sibiya amesema wananchi wanaotekeleza hujuma hizo za kibaguzi na kupora maduka ya wageni hawaliwakilishi taifa zima la Afrika Kusini, bali wanasukumwa na matakwa binafsi.

Hujuma dhidi ya maduka ya wageni mjini Johannesburg

Watu wasipungua 12 wakiwemo Waafrika Kusini wameuawa katika ghasia na hujuma dhidi ya raia wa kigeni nchini Afrika Kusini. Polisi ya nchi hiyo imetangaza kuwa imewatia nguvuni watu 700 kwa kuhusika na ghasia na hujuma hizo.

Tayari mamia ya raia wa Nigeria wameondoka nchini Afrika Kusini na kurejea nchini kwao kwa usafiri uliogharamiwa na serikali yao, kutokana na kushadidi hujuma hizo.