UNICEF: Watoto milioni moja wanakabiliwa na hatari ya kifo nchini Msumbiji
(last modified Wed, 18 Sep 2019 07:50:15 GMT )
Sep 18, 2019 07:50 UTC
  • UNICEF: Watoto milioni moja wanakabiliwa na hatari ya kifo nchini Msumbiji

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, watoto milioni moja nchini Msumbiji wanakabiliwa na hatari ya kifo baada ya nchi hiyo kukumbwa na kimbunga.

Ripoti ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) imeeleza kuwa, roho za watoto milioni moja zipo hatarini kutokana na Msumbiji kukumbwa na vimbunga viwili mtawalia.

Kadhalika taarifa hiyo imebainisha kwamba, vimbunga vilivyoikumba Msumbiji katika miezi ya hivi karibuni vimeacha athari mbaya mno ambapo watoto wasiopungua milioni moja wa nchi hiyo wanakabiliwa na lishe duni.

Sehemu nyingine ya ripoti ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) inasema kuwa, zaidi ya watoto 160,000 walio na umri wa chini ya miaka 5 nchini Msumbuji wanakabiliwa na hali mbaya mno ya lishe duni ikiwa ni matokeo ya athari mbaya za vimbunga vilivyoikumba nchi hiyo.

Mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Idai nchini Zimbabwe

Ofisi ya Uratibu ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Masuala ya Kibinaadamu (OCHA) imetangaza kuwa, zaidi ya watu milioni moja na laki nane na nusu waliathiriwa na kimbunga cha Idai nchini Msumbiji pekee.

Mamia ya watu walipoteza maisha mwezi Machi mwaka huu kutokana na kimbunga kikali cha Idai kilichopiga eneo la kusini mwa Afrika. 

Kimbunga cha Idai mbali na Msumbiji kilizikumba pia nchi za Zimbabwe na Malawi na kusababisha maafa na uharibifu mkubwa. Licha ya kupita miezi kadhaa tangu kutokea kimbunga hicho athari zake bado zinashuhudiwa.