Wamsumbiji washiriki katika uchaguzi muhimu kwa amani na usalama wa nchi yao
(last modified Tue, 15 Oct 2019 08:04:03 GMT )
Oct 15, 2019 08:04 UTC
  • Wamsumbiji washiriki katika uchaguzi muhimu kwa amani na usalama wa nchi yao

Wananchi wa Msumbiji leo wameelekea kwenye vituo vya kupigia kura kushiriki katika uchaguzi unaotazamiwa kupima mafanikio ya makubaliano tete ya amani yaliyosainiwa miezi miwili iliyopita kati ya chama tawala cha Frelimo na hasimu wake wa vita vya muda mrefu vya ndani Renamo, ambayo sasa ni chama cha siasa cha upinzani.

Chaguzi hizo za leo za urais, ubunge na mikoa zinatazamiwa kurefusha utawala wa miongo kadhaa wa chama cha Frelimo katika taifa hilo la kusini mwa Afrika linalotazamiwa kuwa moja ya wauzaji wakubwa wa gesi duniani.

Hata hivyo chama cha Renamo kina matumaini kuwa kitaweza kuyatumia mabadiliko ya sheria ya uchaguzi yaliyoafikiwa katika mkataba wa amani kujinyakulia ushindi kwa mara ya kwanza kwenye ngome zake za jadi katika mikoa ya kati na kaskazini mwa Msumbiji tangu vilipomalizika vita vya ndani kupitia makubaliano ya mwaka 1992.

Wachambuzi na makundi ya kutetea haki yameonya kuwa machafuko yanaweza kutokea endapo Renamo itashindwa kupata ushindi katika maeneo hayo.

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji

Rais Filipe Nyusi ambaye amepiga kura katika skuli moja ya Maputo, mji mkuu wa nchi hiyo amesema: "Msumbiji imechagua amani". Aidha amewapongeza Wamsumbiji kwa kuamua hatima yao kupitia chaguzi na kuwahimiza wananchi hao kwenda kupiga kura kwa amani.

Takribani wapigakura wote milioni 13 waliojiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa leo walizaliwa baada ya Frelimo kuingia madarakani mwaka 1975, wakati Msumbiji ilipojipatia uhuru wake kutoka utawala wa kikoloni wa Ureno.../