Maelfu waandamana Sudan wakitaka kuvunjwa chama cha al-Bashir
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56779-maelfu_waandamana_sudan_wakitaka_kuvunjwa_chama_cha_al_bashir
Maelfu ya wananchi wa Sudan wamejitokeza mabarabarani katika maandamano ya kushinikiza kuvunjiliwa mbali kilichokuwa chama tawala nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 22, 2019 04:36 UTC
  • Maelfu waandamana Sudan wakitaka kuvunjwa chama cha al-Bashir

Maelfu ya wananchi wa Sudan wamejitokeza mabarabarani katika maandamano ya kushinikiza kuvunjiliwa mbali kilichokuwa chama tawala nchini humo.

Maandamano hayo yalishuhudiwa jana Jumatatu katika mji mkuu Khartoum na miji mingine mikubwa nchini humo. Waandamanaji wanataka kutimizwa malengo ya mapinduzi ya Sudan, kukivunja chama tawala cha zamani NCP cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al-Bashir, na kuwafikisha mahakamani viongozi wa zamani waliohusika na mauaji ya waandamanaji mbele ya makao makuu ya jeshi.

Aidha serikali ya mpito ya Sudan na makundi mbalimbali ya upinzani yaliyo chini ya mwavuli wa chama cha Sudan Revolutionary Front, jana yalisaini muafaka wa kisiasa na makubaliano ya kusitisha vita, ikiwa ni maendeleo makubwa yaliyopatikana katika mazungumzo ya sasa ya amani yanayolenga kumaliza mgororo uliodumu kwa miongo kadhaa sasa nchini humo.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ambaye amekuwa mpatanishi kwenye mchakato wa amani nchini Sudan tangu Oktoba 14, amezipongeza pande hizo mbili kwa kufikia makubaliano hayo, na kusema amani na utulivu wa Sudan ni kwa maslahi ya eneo zima.

Rais Salva Kiir sa Sudan Kusini na makundi ya kisiasa ya Sudan

Sudan ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wananchi kuanzia katikati ya mwezi Disemba mwaka jana dhidi ya hali mbaya ya uchumi; na kufuatia ghasia hizo jeshi la Sudan tarehe 11 Aprili mwaka huu lilimpindua madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir na kushika hatamu za uongozi kwa kuunda Baraza la Kijeshi la Mpito. 

Mapema mwezi uliopita, serikali mpya iliapishwa nchini Sudan likiwa ni baraza la kwanza la mawaziri tangu rais huyo wa zamani wa nchi hiyo aondolewe madarakani Aprili mwaka huu.