Putin ataka kuongezeka maradufu mabadilishano ya kibiashara kati ya Russia na Afrika
Rais Vladimir Putin wa Russia ametoa mwito wa kuongezeka maradufu mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi yake na nchi za bara Afrika.
Amesema mabadilishano hayo yaliongezeka mara mbili hadi kiwango cha dola bilioni 20 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, lakini anasisitiza kuwa kuna haja ya mabadilishano hayo kuongezeka hadi dola bilioni 40 katika muda wa miaka minne hadi mitano ijayo.
Rais Putin alitoa mwito huo jana Jumatano katika mkutano wa kiuchumi wa Russia na Afrika utakaomalizika kesho Alkhamisi katika mji wa bandari wa Sochi na kufafanua kuwa, "Naaminia kwamba, tuna uwezo wa angalau kuongeza maradufu kiwango cha mabadilishano ya biashara ndani ya miaka minne hadi mitano ijayo. Russia itafanya kila iwezalo kuziunganisha maeneo ya biashara huru ya Afrika na Muungano wa Uchumi wa Ulaya na Asia (Eurasian Economic Union) kwa kupanua na kufadhili biashara."

Rais Putin ameongeza kuwa, kustawi kwa miamala ya kibiashara ni kwa maslahi ya pande zote na suluhu kwa changamoto nyingi za kijamii. Rais wa Russia anaitakidi kuwa, hivi sasa bara la Afrika limegeuka kuwa bara la fursa nyingi.
Aidha ametilia mkazo kupanuliwa na kustawishwa mashirikiano ya kijeshi na kiufundi pamoja na misaada ya kibinadamu ya Moscow kwa nchi za Afrika.
Mkutano huo wa wa kiuchumi wa Russia na Afrika unatajwa kuwa mkubwa zaidi kati ya pande mbili hizo tangu enzi za Umoja wa Sovieti.