Mahakama Msumbiji yapinga rufaa ya wapinzani kuhusu matokeo ya uchaguzi
Mahakama ya Katiba Msumbiji imetupilia mbali rufaa ya chama cha upinzani cha Renamo ambacho kilikuwa kinataka kufutwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa hivi karibuni.
Katika hukumu yake, Mahakama ya Katiba imesema pingamizi kuhusu ushindi wa Rais Filipe Nyusi na chama chake, Frelimo, katika uchaguzi wa Oktoba 15 inatupiliwa mbali. Mahakama imesema waliowasilisha kesi hawakutoa ushahidi wa kutosha kutilia nguvu madai yao.
Uchaguzi huo wa rais, bunge na serikali za mikoa ulitazamiwa kuyapa nguvu mapatano ya amani yaliyofikiwa baina ya Nyusi na kiongozi wa Renamo Ossufo Momade mwezi Agosti na kuhitimisha miongo minne ya uhasama baina ya vyama hivyo viwili.

Lakini kinyume na ilivyotarajiwa, uchaguzi huo umezidisha uhasama huku wapinzani wakisema kulikuwa na wizi mkubwa wa kura. Momade amesema nchi hiyo ya kusini mwa Afrika huenda ikatumbukia tena katika vita vya ndani iwapo matokeo ya uchaguzi yataidhinishwa.