Algeria wazidi kuandamana kupinga uchaguzi unaowashirikisha watu wa Bouteflika
Barabara za Algeria zimeendelea kushuhudia maandamano makubwa ya wananchi kwa wiki ya 37 wanaolalamikia mfumo wa utawala wa nchi hiyo na kutofuatiliwa mafisadi wa utawala wa Abdelaziz Bouteflika.
Shirika la habari la Fars limeripoti kuwa, wananchi wa Algeria jana Ijumaa walimiminika kwenye barabara na mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo Algiers wakishinikiza kufutwa kazi wafuasi wote wa Abdelaziz Boteflika, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyelazimishwa kujiuzulu na maandamano makubwa ya wananchi.
Waandamanaji wamepiga mayowe ya kupinga kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo kutokana na kuwashirikisha mabaki ya utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo.
Maandamano ya jana yalikuwa ya wiki ya 37 mfululizo ya wananchi hao ambao kila Ijumaa wanafanya maandamano ya kushinikiza kufutwa kazi na kufuatiliwa kisheria mafisadi wa utawala wa Abdelaziz Bouteflika.
Uchaguzi wa rais wa Algeria ambao utakuwa wa kwanza tangu kujiuzulu Bouteflika unatarajiwa kufanyika tarehe 12 mwezi ujao wa Disemba.
Maandamano ya wananchi wa Algeria yalianza baada ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika kutangaza mwezi Februari 2019 kwamba atagombea tena urais katika uchaguzi wa nchi hiyo.
Kupenda mno madaraka rais huyo mgonjwa kuliwakasirisha mno wananchi wa Algeria na kuamua kumiminika barabarani na kufanikiwa kumlazimisha rais huyo kujiuzulu. Hata hivyo wananchi hao wanasema kuwa mapinduzi yao yamepinduliwa, na mafisadi wa utawala wa Bouteflika wanaendelea kushika nyadhifa muhimu na nyeti nchini Algeria, ndio maana wanaendelea na maandamano yao ya kila Ijumaa.