Uchaguzi wa rais Algeria kufanyika bila kuhudhuriwa na waangalizi wa kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57522-uchaguzi_wa_rais_algeria_kufanyika_bila_kuhudhuriwa_na_waangalizi_wa_kimataifa
Msemaji wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Algeria amesema, hakutakuwepo na waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika tarehe 12 ya mwezi ujao wa Desemba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 27, 2019 00:13 UTC
  • Uchaguzi wa rais Algeria kufanyika bila kuhudhuriwa na waangalizi wa kimataifa

Msemaji wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Algeria amesema, hakutakuwepo na waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika tarehe 12 ya mwezi ujao wa Desemba.

Ali Dhira ameongeza kuwa, Algeria ni nchi huru inayojitawala na inatekeleza wajibu wake kikamilifu, hivyo haitasubiri asasi au mwangalizi yeyote yule.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa uchaguzi mkuu wa Algeria kufanyika bila ya kuhudhuriwa na waangalizi wa kimataifa.

Tangu ulipofanyika uchaguzi wa Bunge mwaka 2012, viongozi wa Algeria wamekuwa kila mara wakiwaalika waangalizi wa kimataifa kushiriki katika uangalizi wa mchakato wa chaguzi za nchi hiyo iwe ni wa bunge au rais; na aghalabu ya waangalizi hao ni kutoka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.

Aliyekuwa rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika

Uchaguzi wa rais wa Desemba 12 utakuwa wa kwanza kufanyika nchini humo tangu aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika alipolazimika kung'atuka madarakani Aprili Pili mwaka huu kutokana na maandamano ya upinzani ya wananchi.

Wakati huohuo maandamano ya upinzani yanaendelea kufanyika nchini Algeria kutaka viongozi na maafisa wote wa serikali waliohudumu katika utawala wa Bouteflika waondoke madarakani kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais.../