Algeria yaendelea kushuhudia maandamano sambamba na kukaribia kufanyika uchaguzi wa Rais
Mji mkuu wa Algeria, Algiers na miji mingine ya nchi hiyo imeendelea kushuhudia maandamano makubwa ya wapinzani zikiwa zimebakia siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi wa Rais nchini humo.
Jana Ijumaa Algeria ilishuhudia maandamano kwa wiki ya 41 mtawalia ambapo waandamanaji hao walitangaza tena msimamo wao wa kupinga kufanyika uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo tarehe 12 ya mwezi ujao wa Disemba. Waaandamanaji wanataka viongozi na maafisa wote wa serikali waliohudumu katika utawala wa Rais wa zamani Abdelaziz Bouteflika waondoke madarakani kabla ya kufanyika uchaguzi huo.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara za kutaka kuchukuliwa hatua mafisadi na kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa.
"Tunaapa kwamba, uchaguzi hautafanyika, hii ni nchi yetu na sisi ndiyo tunaopaswa kuchukua maamuzi kuhusu hatima ya nchi", hizo ni baadhi tu ya nara zilizokuwa zikipigwa na waandamanaji hao wenye hasira nchini Algeria.
Vikosi vya usalama vya Algeria vikiwa vimejizatiti kikamilifu kwa silaha na magari washawasha viliingilia kati na kuwatawanya waandamanaji hao huku vikiwatia mbaroni baaadhi yao.
Uchaguzi wa Rais wa Desemba 12 nchini Algeria utakuwa wa kwanza kufanyika nchini humo tangu aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika alipolazimika kung'atuka madarakani Aprili Pili mwaka huu kutokana na maandamano ya upinzani ya wananchi.