Rais Kiir wa Sudan Kusini na Machar kukutana ana kwa ana Juba
Mahasimu wa kisiasa nchini Sudan Kusini, Rais Salva Kiir na kiongozi wa upinzani, Riek Machar wanatazamiwa kukutana leo Jumanne katika mazungumzo ya uso kwa uso katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba.
Hayo yamethibitishwa na Naibu Msemaji wa vikosi vya upinzani katika mahojiano na idhaa ya Tamazuj ambaye ameongeza kuwa, wawili hao wanatazamiwa kujadili nukta muhimu juu ya muundo wa serikali ya muungano wa kitaifa.
Amesema miongoni mwa yale yatakayojadiliwa kwenye kikao cha leo ni kuhusu idadi na majimbo na mipaka yake, ambayo yaliyoongezwa hadi 32 kupitia dikrii ya Rais Kiir.
Aidha nukta nyingine ya utata ambayo inatazamiwa kuzungumziwa ni suala la kuwajumuisha askari waasi kwenye jeshi la taifa, kadhia ambayo imekuwa na mvutano kati ya pande mbili hizo hasimu kwa muda mrefu.
Umoja wa Afrika umewapa Rais Salva Kiir na kiongozi wa upinzani, Riek Machar nafasi ya mwisho ya siku 100 ya kuunda serikali ya pamoja, baada ya kushindwa kufanya hivyo tarehe 12 mwezi Novemba mwaka huu.
Haya yanaripotiwa siku chache baada ya watu 67 kuuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika mapigano mapya ya kikabila yaliyotokea katika jimbo la Western Lakes katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.