Mji mkuu wa Sudan washuhudia maandamano makubwa
Maelfu ya wananchi wa mji mkuu wa Sudan Khartoum jana waliandamana wakitaka kupatiwa ufumbuzi matatizo ya kiuchumi na kupatikana uadilifu katika nchi hiyo.
Maandamano hayo yamefanyika wiki moja tu baada ya maadhimisho ya mwaka wa kwanza tangu kuanza maandamano ya wananchi yaliyopelekea kuondolewa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara za kudai uadilifu na kisha wakaenda kukusanyika mbele ya ikulu ya rais.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba pia picha za baadhi ya wananchi waliouawa katika maandamano ya wananchi mwaka jana wamesema, serikali iliyoko madarakani inapaswa kuboresha hali ya uchumi wa nchi hiyo.
Sudan ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wananchi tarehe 19 Disemba mwaka jana dhidi ya hali mbaya ya uchumi; na kufuatia ghasia hizo jeshi la Sudan tarehe 11 Aprili mwaka huu lilimpindua madarakani rais huyo wa zamani na kushika hatamu za uongozi kwa kuunda baraza la kijeshi, ambalo nalo baadaye lilivunjwa baada ya kuundwa serikali ya mpito.
Serikali mpya ya Sudan iliyoko madarakani hivi sasa inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kuboresha uchumi wa nchi hiyo uliosambaratika vibaya, kupambana na ufisadi uliokita miziz, na kuandaa mazingira bora na mazuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki.