Umoja wa Mataifa wapongeza hatua ya Machar kurejea Juba
Umoja wa Mataifa umepongeza hatua ya Riek Machar, kiongozi wa upinzani wa Sudan Kusini kurejea katika mji mkuu wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika na kuunda serikali na Rais Salva Kiir.
Herve Ladsous, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na vikosi vya kulinda amani vya umoja huo alimeliambia Baraza la Usalama la UN kuwa, hatua ya Machar kurejea nchini na kuunda serikali na hasimu wake Salva Kiir inaashiria mwamko na mwanzo mpya wenye matumaini. Ladsous amesema kuwa, "Ni muhimu sana kwa pande husika kutumia fursa hii kuonyesha namna walivyojitolea kutekeleza makubaliano ya amani.”
Balozi Msaidizi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa, Joseph Mourn Malok kwa upande wake amesema serikali mpya inatarajiwa kuundwa baada ya majadiliano ya pande husika katika kipindi cha siku moja au mbilli hivi.
Jana Jumanne, Machar aliwasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba na kuapishwa kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo katika serikali inayoongozwa na hasimu wake wa muda mrefu, Rais Salva Kiir.
Kwa mujibu wa mapatano ya amani yaliyotiwa saini Addis Ababa Ethiopia, kutakuwa na serikali ya mpito itakayodumu kwa muda wa miezi 30. Kiir atachukua asilimia 53 ya viti serikalini huku upande wa Machar ukipata asilimia 33 na wafungwa wa zamani wa kisiasa na vyama vingine vya kisiasa vikipata asilimia 7 kila mmoja.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.