Waziri Mkuu wa Sudan aunda tume ya kuchunguza ukandamizaji dhidi ya raia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59319-waziri_mkuu_wa_sudan_aunda_tume_ya_kuchunguza_ukandamizaji_dhidi_ya_raia
Waziri Mkuu wa Sudan ametangaza kuwa ameunda tume ya kuchunguza vitendo vya ukandamizaji vilivyofanywa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo Alkhamisi na Ijumaa ya jana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 22, 2020 09:11 UTC
  • Waziri Mkuu wa Sudan aunda tume ya kuchunguza ukandamizaji dhidi ya raia

Waziri Mkuu wa Sudan ametangaza kuwa ameunda tume ya kuchunguza vitendo vya ukandamizaji vilivyofanywa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo Alkhamisi na Ijumaa ya jana.

Akizungumza kwa njia ya televisheni, Abdalla Hamdok amesema kuwa: Nimechukua uamuzi wa kuunda kamati ya uchunguzi kufuatia matukio ya siku mbili zilizopita.

Waziri Mkuu Hamdok amesema kuwa, Mwanasheria Mkuu Taj-Elsir Ali ataongoza kamati hiyo ya uchunguzi ambayo inapaswa kutoa ripoti yake katika kipindi cha siku saba zijazo.

Maeneo yaliyoshuhudiwa maandamano makubwa zaidi Alkhamisi na Ijumaa ya jana ni mji mkuu Khartoum. Vikosi vya usalama siku ya Alkhamisi vilivamia maandamano ya wananchi hao na kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi ambapo kwa akali watu 17 walijeruhiwa.

Raia hao walikuwa wakiandamana dhidi ya Baraza la Utawala linaloongozwa na Luteni Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan.

Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan

Hivi karibuni Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan, Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alikutana na kufanya mazungumzo huko nchini Uganda na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hatua hiyo imekosolewa vikali na ukosoaji huo umekuwa ukiongezeka kila siku nchini Sudan. Serikali ya Khartoum inasema kuwa, al-Burhan alikutana na Netanyahu bila ya kushauriana na serikali.

Hivi karibuni kundi la mawakili nchini humo liliandaa faili la mashtaka ya jinai dhidi ya Luteni Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan Kiongozi wa Baraza la Utawala la Sudan kutokana na kiongozi huyo kukiuka sheria inayotaka kususiwa Israel.