Apr 28, 2016 04:07 UTC
  • Waandamanaji  Afrika Kusini wamtaka Rais Zuma ajiuzulu

Wapinzani nchini Afrika Kusini wameitisha maandamano ya kumshinikiza Rais Jacob Zuma ajiuzulu.

Watu hao wakiongozwa na mashirika 75 ya kiraia, wametoa matakwa hayo kufuatia uamuzi uliotolewa tarehe 31 Machi na mahakama ya katiba, unaosema kuwa Rais Zuma hakufuata mapendekezo ya msimamizi wa mali za umma ya kumtaka kulipia gharama za ukarabati wa nyumba yake binafsi huko Nkandla, KwaZulu-Natal, kitendo ambacho kinadaiwa kukiuka katiba. Maandamano yamefanyika nchini kote siku ya Jumatano ikiwemo mjini Johannesburg, Cape Town na Durban. Mjini Johannesburg, mamia ya waandamanaji wakiwemo wasomi, wanasiasa, walinzi wa mazingira, wanafunzi, wafanyabiashara na wanaharakati wa kijamii wameshiriki kwenye maandamano hayo wakimtaka rais Zuma ajiuzulu.

Hayo yanajiri wakati ambao chama tawala cha ANC nchini Afrika Kusini kimetoa taarifa na kutangaza kuwa, matamshi ya Julius Malema mmoja wa wapinzani wa Rais Jacob Zuma ni hiana na usaliti dhidi ya maslahi ya kitaifa na kwamba, serikali ya nchi hiyo itamshtaki. Julius Malema kiongozi wa upinzani nchini Afrika Kusini ametishia kwamba, ili kuiondoa madarakani serikali ya Zuma yuko tayari kutumia nguvu na hata ikibidi atabeba silaha. Malema ambaye ni mkuu wa chama cha Economic Freedom Fighters anamtuhumu Rais Zuma kwa ubadhirifu na anataka kiongozi huyo auzuliwe madarakani.

Tags