Magaidi 129 wameuawa ndani ya mwezi mmoja na maafisa usalama Msumbiji
(last modified Wed, 29 Apr 2020 11:12:30 GMT )
Apr 29, 2020 11:12 UTC
  • Magaidi 129 wameuawa ndani ya mwezi mmoja na maafisa usalama Msumbiji

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji ametangaza habari ya kuuawa makumi ya wanachama wa magenge ya kigaidi kaskazini mwa nchi katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Amade Miquidade alisema hayo jana katika taarifa na kuongeza kuwa, maafisa usalama wa nchi hiyo walifanikiwa kuwaangamiza magaidi hao katika operesheni tofauti zilizofanyika baina ya Aprili 7 na Aprili 13 katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado.

Amesema 39 miongoni mwao waliuawa walipojaribu kuvamia kijiji cha Muidumbe mnamo Aprili 7, huku 59 wakiuawa katika majibizano ya risasi na maafisa usalama katika kisiwa cha Querimba mkoani hapo siku tatu baadaye.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Msumbiji imeongeza kuwa, wanachama wengine 31 waliuawa katika operesheni zilizofanyika baina ya Aprili 11 na Aprili 13 katika kisiwa cha Ibo, na kwamba operesheni hizo zilikuwa za kulipiza kisasi cha kuuawa makumi ya wanakijiji katika mkoa huo mapema mwezi huu.

Askari akitathmini kijiji kilichovamiwa na magaidi mkoani Cabo Delgado

Hivi karibuni, msemaji wa polisi ya Msumbiji, Orlando Modumane alisema wanakijiji 52 waliuawa na wanachama wa genge la kigaidi baada ya kukataa kusajiliwa kujiunga na kundi hilo mnamo Aprili 7 katika kijiji cha Xitaxi wilayani Muidumbe, katika mkoa huo ambao unaendelea kushuhudia harakati za kigaidi kwa muda sasa wa Cabo Delgado, kaskazini mwa nchi.

Vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017 vimekuwa vikishuhudia mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shaabab.