Safari ya Jenerali Haftar nchini Misri
(last modified Thu, 04 Jun 2020 07:49:59 GMT )
Jun 04, 2020 07:49 UTC
  • Safari ya Jenerali Haftar nchini Misri

Kamanda wa kundi linalojiita Jeshi la Kitaifa la Libya yuko mjini Cairo Misri, kwa lengo la kuonana na kuzungumza na viongozi wa nchi hiyo.

Lengo la safari hiyo limetajwa kuwa ni kuratibu na kufanya mashauriano na viongozi wa Misri kuhusiana na matukio ya karibuni huko Libya.

Wakati huo huo mazungumzo yamefanyika huko Moscow kati ya Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, ambao ni upande wa pili wa mapigano ya ndani nchini Libya.

Mohamed Taher Siala, Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya amesema kwamba katika mazungumzo yake na Lavrov pamoja na naibu wake Mikhail Bogdanov, wamezungumza na kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi karibuni huko Libya.

Mashambulio ya askari wa Haftar katika makazi ya raia

 

Askari wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar tokea mwezi Aprili 2019 wamekuwa wakiushambilia kwa makombora na mizingi mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa lengo la kuudhibiti mji huo na kuutoa mikononi mwa serikali halali inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj.

Mapambano makali ambayo yamekuwa yakionyeshwa na askari wa serikali hiyo yamefelisha njama na hujuma zote ambazo zimekuwa zikifanywa dhidi ya mji mkuu huo kwa msaada wa nchi za Magharibi na Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia, Imarati na Misri.

Nchi tatu hizo za Kiarabu zikisaidiwa kwa karibu na Ufaransa zinawasaidia kijeshi askari wa Haftar nazo Uturuki, Italia, Qatar na Umoja wa Mataifa zikiiunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyo na makao makuu yake mjini Tripoli.

Tags