Jun 10, 2020 05:24 UTC
  • Mahakama ya Kimataifa ya Jinai yamkamata kiongozi wa Janjaweed

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetangaza kuwa, kiongozi wa wanamgambo wa Janjaweed Ali Kosheib ambaye alikuwa mtu wa karibu kwa rais wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir amejisalimisha kwa mahakama hiyo na kwamba anakabiliwa na tuhuma za kutenda jinai za kivita katika jimbo la Darfur huko magharibi mwa Sudan tangu mwaka 2003.

Taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo imesema kuwa, Ali Kosheib anashikiliwa na mahakama ya ICC baada ya kujisalimisha mwenyewe katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa mujibu wa waranti wa kutiwa kwake nguvuni uliokuwa umetolewa na mahakama hiyo Aprili mwaka 2007.

Mahakama ya ICC pia imezishukuru nchi zote zilizofanikisha zoezi hilo ikiwemo Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati na kusema kuwa, mtuhumiwa huyo atasimamishwa kizimbani hivi karibuni.

Jamhuri ya Afrika ya Kati imetangaza kuwa Ali Kosheib amekamatwa katika mji wa Birao na kwamba alisafirishwa mapema jana kwa ndege kuelea The Hague huko Uholanzi kwenye makao ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Inaaminika kwamba Ali Kosheib alikuwa kiunganishi baina ya vinara wa kundi la Janjaweed na utawala wa Omar al Bashir. Wendesha mashtaka wanasema aliongoza kundi la wanamgambo wa Janjaweed waliofanya mashambulizi dhidi ya vijiji vya Darfur na kufanya jinai za mauaji, ubakaji wa wanawake, uporaji wa mali na kutesa raia baina ya mwaka 2003 hadi 2004.

Maelfu ya watu waliuawa katika hujuma za Janjaweed huko Darfur.

Ali Kosheib ndiye mtuhumiwa wa kwanza Msudan kufikishwa katika mahakama ya Kimataifa ya Jinai na anashika nafasi ya nne katika orodha ya watuhumiwa wakuu wa jinai za vita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanyika Darfur. Orodha hiyo inaongozwa na aliyekuwa rais wa Sudan, Omar al Bashir, waziri wake wa ulinzi Abdulraheem Mohammed Hussein na aliyekuwa waziri wake wa mambo ya ndani Ahmad Haroun.   

Tags