Jun 21, 2020 14:53 UTC
  • Mashambulizi pacha ya mabomu yaua raia na askari kadhaa nchini Somalia

Kwa akali watu saba wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya mabomu yanayoaminika kufanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab huko kusini na katikati mwa Somalia ndani ya masaa 24.

Duru za kiusalama zimethibitisha leo Jumapili kutokea mashambulizi hayo mawili yanayoaminika kuwa ya kigaidi. Katika shambulizi la kwanza, mabomu mawili yaliyotegwa nje ya nyumba ya afisa wa jeshi katika mji wa Wanlaweyn, yapata kilomita 90 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu yaripuka na kuua watu wanne wakiwemo wanajeshi na raia.

Katika hujuma ya pili iliyojiri mapema leo, magaidi watatu wanaosadikika kuwa wanachama wa al-Shabaab walitekeleza shambulizi la kujiripua kwa mabomu katika kituo cha upekuzi katika mji wa Bacadweyn ulioko katika jimbo la Galmudug, katikati mwa nchi.

Meja Abdullahi Ahmed, afisa wa jeshi katika mji jirani wa Galkayo amethibitisha kutokea shambulizi hilo na kusema kuwa limeua wanajeshi watatu na kujeruhi wengine kadhaa.

Wakazi wa mji wa Bacadweyn, umbali wa kilomita 180 kusini mwa mji wa Galkayo wanaamini kuwa shambulizi hilo limefanywa na wanachama wa al-Shabaab.

Wanamgambo wa al-Shabaab wanaofanya jinai za kutisha ndani na nje ya Somalia

Mapema mwezi huu, Jeshi la Taifa la Somalia lilitangaza kuwa limefanikiwa kuua wanachama 37 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika mji wa Hudur, eneo la Bakol huko kusini mwa nchi.

Kundi la kigaidi a kitakfiri la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah limehusika na mashambulizi mengi ndani ya Somalia na katika nchi jirani tokea mwaka 2007.

Tags