Serikali ya Nigeria yaendelea na hatua kandamizi dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky
Mtoto wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, serikali ya Rais Buhari imeendelea kufanya vitendo vya ukandamizaji dhidi ya baba yake huyo anayeshikiliwa gerezani.
Muhammad Ibrahim Zakzaky akizungumzia jinai zilizofanywa na serikali ya Nigeria dhidi ya familia yake na Harakati yay Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, serikali ya nchi hiyo imewaua watoto sita wa Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Kuhusiana na afya ya Sheikh Zakzaky, Muhammad Ibrahim Zakzaky amesema kuwa, hali ya kiafya ya baba yake bado hairidhishi na kwamba, uwezo wake wa kuona unapungua siku baada ya siku.
Hatua kandamizi na za kikatili za polisi na jeshi la Nigeria dhidi ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky zingali zinaendelea na hadi sasa idadi kubwa ya wafuasi wa kiongozi huyo wa kidini wamewekwa kizuizini au wameuawa shahidi.
Makumi ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na kiongozi huyo wa harakati hiyo wamewekwa kizuizini tangu walipotiwa nguvuni mwaka 2015 baada ya jeshi la Nigeria kushambulia Husainia ya mji wa Zaria jimboni Kaduna; na tangu wakati huo hadi sasa wanaendelea kusota jela pasi na kuthibitishiwa makosa na mashtaka yanayowakabili.
Mahakama Kuu ya Nigeria iliwahi kutoa hukumu iliyosisitiza kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe hawana hatia yoyote na ikaamuru waachiliwe huru, lakini wawili hao wangali wanaendelea kuwekwa jela na hivi sasa hali zao za afya ni mbaya sana.