Kenya ni nchi ya kwanza Afrika kusambaza intaneti kupitia baluni
Kenya imekuwa nchi ya kwanza kutoa huduma za inteneti kupitia baloni (puto) na hivyo kuwawezesha maelfu ya watu nchini humo kupata huduma za intaneti kirahisi.
Baloni hizo ambazo zinaenda kilomita 18 juu katika anga ya kati (stratosphere), juu zaidi ya eneo ambalo hurukia ndege za abiria, ziitatoa huduma za intaneti za mfumo wa 4G LTE na zitasambaza itaneti katika eneo lenye ukubwa wa maili mraba 31,000 katika eneo la kati na magharibi mwa Kenya, ukiwemo mji mkuu, Nairobi.
Huduma huyo iliyozinduliwa Jumanne inatolewa na shirika la Loon, ambalo linamilikiwa na Shirika la Google. Shirika hilo kwa kuanzia linatumia baloni 35 katika mradi huo ambapo majaribio yamefanyika kwa miezi kadhaa sasa na ambao unafanyika kwa ushirikiano na Shirika la Simu la Telkom Kenya. Huduma ya intaneti kwa kutumia baloni imewahi kutumika maeneo mengine duniani lakini wakati wa dharura tu mfano ukiwa ni Puerto Rico mwaka 2017 baada ya kimbunga kuharibu milingoti ya mashirika ya simu za mkononi.
Shirika la Loon linasema huduma hiyo ya intaneti kupitia baloni zilizo katika anga ya kati si ghali na hufukisha intaneti katika maeneo ambayo hayana miundo msingi ya itaneti. Hatahivyo wakosoaji wanasema Kenya haihitajii mradi huo kwani idadi kubwa ya Wakenya wanapata huduma za intaneti. Kwa mujibu wa uchunguzi, Wakenya milioni 39 kati ya milioni 48 wanapata huduma za intaneti, hiki kikiwa ni kiwango cha juu sana ikilinganishwa na aghalabu ya nchi zinazostawi duniani. Shirika la Loon linasema limezindua mradi huo nchini Kenya kutokana na hamu ya nchi hiyo kukumbatia teknolojia mpya.
Baloni inayotumwa katika anga ya kati kutoa huduma za intaneti hurejea ardhini baada ya siku 100.