Polisi ya Misri wahujumu chama cha waandishi habari
Polisi nchini Misri wamevamia idara ya waandishi habari mjini Cairo na kuwatia mbaroni waandishi habari wawili wanaotuhumiwa kuchochea maandamano dhidi ya serikali.
Waandishi habari waliokamatwa ni Amr Badr na Mahmud el Sakka ambao wanaiandikia tovuti ya upinzani ya Bawabet Yanayer (Lango la Januari). Jina la tovuti hiyo linanasibishwa na mwamko wa wananchi wa mwaka 2011 uliopelekea kuangushwa utawala wa kiimla wa dikteta Hosni Mubarak.
Maandamano yanaendelea kote nchini Misri kupinga hatua ya Rais Abdel Fattah el Sisi kuipa Saudi Arabi visiwa viwili vya Misri vya Sanafir na Tiran katika Bahari ya Sham
Wakati wa safari ya Mfalme Salman wa Saudi Arabia nchini Misri siku chache zilizopita, serikali ya Misri ilitangaza rasmi kutiwa saini makubaliano ya mipaka ya baharini kati ya nchi hiyo na Saudi Arabia; na kwa mujibu wa makubaliano hayo, Misri imeipatia Saudia visiwa viwili vya Sanafir na Tiran. Tangazo hilo la kushtukiza limeamsha hasira na malalamiko ya Wamisri ambao walikuwa wakivitambua visiwa hivyo kuwa ni ardhi yao kwa miongo mingi.
Wananchi wa Misri wameikosoa na kuipinga vikali serikali kwa hatua yake ya kusaini makubaliano hayo na serikali ya Riyadh.
Wanaharakati mbalimbali nchini Misri wametoa maoni wakisema kuwa Rais al Sisi anauza ardhi ya Misri kwa muitifaki tajiri kupitia mapatano ya udhalilishaji.