Amnesty: Msumbiji inawatesa na kuwanyanyasa washukiwa wa vitendo vya uasi
(last modified Thu, 10 Sep 2020 06:47:56 GMT )
Sep 10, 2020 06:47 UTC
  •  Amnesty: Msumbiji inawatesa na kuwanyanyasa washukiwa wa vitendo vya uasi

Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, limetangaza kuwa askari jeshi wa serikali ya Msumbiji wanawatesa wanamgambo wanaoshukiwa kufanya mashambulizi katika mkoa wa Cabo Delgado nchini humo. 

Amnesty International jana liliwatuhumu askari jeshi wa  serikali ya Msumbiji kwamba wanawatesa wanachama wa kundi moja la uasi linalobeba silaha katika mkoa wa Cabo Delgado kaskazini mwa nchi hiyo na kwamba kuna uwezekano wanajeshi hao wamefanya mauaji ya kiholela dhidi ya wanachama hao na kuzika maiti nyingi katika makaburi ya umati.  

Mkurugenzi wa Amnesty International katika eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika Deprosa Muchena amesema: "Tabia hii inakinzana na misingi ya ubinadamu. Uhalifu unaofanywa na kundi la al Shabab hauwezi kuhalalisha vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu wa askari jeshi wa Msumbiji". Ameongeza kuwa, serikali ya Msumbiji sasa inapasa kuamuru kufanyike uchunguzi wa wazi, haraka na usioegemea upande wowote ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wahusika wa jinai hizo. 

Kundi hilo la uasi lilianzia harakati zake katika mkoa wa Cabo Delgado unaopakana na Tanzania kwa upande wa kaskazini na Bahari ya Hindi kwa upande wa mashariki  mwezi Oktoba mwaka 2017. Hadi kufikia sasa watu zaidi ya 1000 wameuawa wengi wao wakiwa ni waasi.

Mkoa wa Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji ambayo ni ngome ya kundi la waasi wenye silaha 

Kundi hilo linalobeba silaha aidha limezidisha mashambulizi katika mwaka huu wa 2020, na mwezi Agosti liliuteka mji wa kistratejia wa bandari wa Mocimboa da Praia na kuushikilia kwa karibu mwezi mmoja. 

Orlando Mudumane Msemaji wa Polisi ya Msumbiji amesema kuwa hawana chochote cha kueleza kuhusu tuhuma hizo za Amnesty International.