Kadhaa wauawa katika shambulizi la kigaidi kaskazini mwa Msumbiji
Watu wasiopungua watano wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa vibaya katika shambulio la kigaidi katika jimbo la Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji.
Hayo yalisemwa na polisi ya nchi hiyo jana Jumatano, ambapo imelibebesha dhima ya shambulio hilo kundi la wanamgambo wenye silaha la Naprama.
Orlando Mudumane, Msemaji wa Polisi ya Msumbiji amewaambia waandishi wa habari kwamba, wapiganaji wa Naprama walivamia kijiji cha Ntotue wilayani Mocimboa da Prala na kuwafyatulia risasi raia. "Wakati tunafika kijijini tuligundua kuwa takriban watu watano wameuawa huku wengine wakijeruhiwa vibaya na wengi walikimbia."
Naprama, iliyoanzishwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 16 nchini Msumbiji katika miaka ya 1980, mara nyingi hutazamwa kama wanamgambo wa kijamii. Hivi karibuni limeibuka tena, huku polisi wakihusisha kundi hilo na wimbi la matukio ya ghasia.
Kwa miaka mingi sasa, askari wa serikali na magenge ya waasi na wanamgambo wamekuwa wakikabiliana katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Uasi wa kutumia silaha, ambao chimbuko lake limedaiwa kuwa ni umasikini, uliibuka kaskazini mwa Msumbiji mwaka 2017, na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine kuyahama makazi yao. Zaidi ya watu 100,000 wamekimbia makazi yao kufuatia mashambulizi ya makundi yenye silaha.