Rais wa Algeria asisitizia udharura wa kuundwa taifa huru la Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63608-rais_wa_algeria_asisitizia_udharura_wa_kuundwa_taifa_huru_la_palestina
Kwa mara nyingine tena, Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria amesisitiza kuwa, nchi yake iko pamoja na wananchi madhulumu wa Palestina na kwamba itaendelea kusimama nao hadi pale watakapofanikiwa katika malengo yao matukufu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 24, 2020 03:41 UTC
  • Abdelmadjid Tebboune
    Abdelmadjid Tebboune

Kwa mara nyingine tena, Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria amesisitiza kuwa, nchi yake iko pamoja na wananchi madhulumu wa Palestina na kwamba itaendelea kusimama nao hadi pale watakapofanikiwa katika malengo yao matukufu.

Rais Tebboune alisema hayo jana Jumatano katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya video katika Mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) na kuongeza kuwa, haki isiyopingika ya Wapalestina kuwa na taifa huru, mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu si kitu cha mjadala.

Huku akiashiria kuwa kadhia ya Palestina ni katika sera madhubuti za nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika, Rais wa Algeria amesema, "tutaendelea kuwa waungaji mkono wa Palestina na Wapalestina ambao wanapambana na kikosi katili cha kikoloni, hadi pale taifa lao litakapokuwa huru."

Rais Tebboune amesema kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Palestina, ndiyo njia pekee ya kuleta amani ya kudumu katika eneo la Asia Magharibi.

Usaliti wa Imarati na Bahrain mkabala wa Palestina umelaaniwa katika kona tofauti za dunia

Siku chache kabla ya hotuba hiyo, Rais huyo wa Algeria alisisitiza kuwa, nchi yake inapinga vikali hatua zozote zile zenye lengo la kuanzisha uhusiano na utawala vamizi wa Israel unaotenda jinai kila leo dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Amesema nchi yake katu haitakuwa sehemu ya makubaliano ya kuufanya wa kawaida uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba, inakosoa vikali hatua ya Imarati na Bahrain ya kuanzisha uhusiano na Wazayuni maghasibu.