Buhari ataka kukomeshwa maandamano, machafuko yaendelea Abuja
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ametoa wito wa kukomesha machafuko na maandamano yanayoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo kufuatia mauaji ya raia waliokuwa wakiandamana kupinga ukatili wa polisi.
Machafuko makubwa yalishuhudiwa tena jana katika mji mkubwa zaidi wa Nigeria, Abuja, huku milio ya risasi na moto vikitawala katika jela kuu ya mji huo.
Akihutubia taifa jana kwa mara ya kwanza baada ya kuanza machafuko hayo, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amewahimiza vijana kusitisha maandamano ya mitaani na kushirikiana na serikali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyopo.
Vilevile ameitaka jamii ya kimataifa kufanya juhudi za kujua uhakika wa mambo badala ya kuharakia kutoa hukumu.
Machafuko makubwa ya sasa nchini Nigeria yaliibuka Jumatano iliyopita baina ya askari usalama na raia wanaoandamana ambao walijizatiti kwa silaha baridi.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeripoti kuwa makumi ya watu wameuawa hadi sasa nchini Nigeria kwa kupigwa risasi na polisi wa nchi hiyo.
Amri ya kutotoka nje imetangazwa katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo ili kudhibiti maandamano na machafuko yanayoendelea kwa zaidi ya wiki mbili.

Raia wa Nigeria wamekuwa wakiandamana kote nchini humo wakipinga ukatili unaofanywa na Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (SARS).
Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat amelaani vurugu zinazoendelea nchini Nigeria
Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kukomeshwa kile alichokiita “ukatili” wa polisi nchini Nigeria, nchi ambayo imekumbwa na maandamano kwa wiki mbili sasa.